General

Wazee Wakumbatia Mchezo Wa Mpira Wa Voliboli


Mazoezi yana umuhimu mwingi sana katika mwili wa mwanadamu. Wazee katika mji wa Nyahururu wamekumbatia uchezaji wa voliboli kama njia ya kufanya mazoezi kwa sababu kibao.

Fred Osongo ambaye ni Kocha wa timu ya voliboli mjini Nyahururu anaeleza kuwa yeye na wenzake waliamua kuanzisha mchezo wa voliboli mnamo mwaka juzi. Walianza wakiwa wachezaji wachache lakini kufikia sasa, wamefika wachezaji 40.

Fred anaendelea kusema kuwa sababu kuu iliyowafanya kuanzisha mchezo huu ni haja ya kufanya mazoezi baada ya kazi nyingi za kila siku.

‘Sababu kuu iliyotufanya kuanzisha mchezo huu ni kwa sababu ya kufanya mazoezi baada ya kazi kuona kuwa baadhi yetu ni wanabodaboda. Tulipokuwa tukianzisha mchezo huu, tulikuwa wachache sana. Baadhi ya watu walikuwa na mtazamo kuwa mchezo huu ni wa vijana pekee. Wanaume wengi hawakuwa na hamu ya kutuunga mkono katika mchezo huu kwa vile wengi walichukulia kuwa wanaopaswa kucheza ni vijana pekee. Kufikia sasa tumeweza kuvutia wazee wengi na hivi sasa tuko arobaini,’ Anaeleza.

Fred
anaendelea kusema kuwa mchezo huu umewasaidia sana katika kupunguza uzito wa mwili ili kupigana na magonjwa yanayotokana na uzito wa mwili uliozidi kama kisukari, msisimko wa damu na mengine mengi. Isitoshe, mchezo huu wa voliboli umewasaidia kupata ujuzi mwingi kuhusu sheria za mchezo huu wa wavu.

‘Voliboli imetusaidia sana kwa sababu tumeweza kupata ujuzi mwingi kuhusu uchezaji kwa voliboli na pia unasaidia kupunguza uzito kupita kiasi wa mwili ili kupigana na magonjwa yanayotokana na uzito iliokidhiri wa mwili,’ anaeleza.

Brian ambaye ni mchezaji wa voliboli anaeleza kuwa umuhimu mkubwa wa mchezo huu wa voliboli ni kuwa huwa haitaji nguvu nyingi wakati wa kucheza hivyo huwa rahisi kuchezwa na wazee. Anaongeza kusema kuwa mchezo huu umesaidia kuleta wazee pamoja hivyo kuendeleza ushirirkiano baina yao.

‘Umuhimu wa mchezo huu ni kuwa huwa hauhitaji nguvu nyingi sana kama mchezo wa kandanda wakati wa kucheza hivyo unatufaa sana hasa wazee wa umri wetu. Pia mchezo huu umetusaidia kuja pamoja na kujuana na h
ili limetusaidia kuunda urafiki kiasi cha kwamba tunaweza kusaidiana iwapo mmoja wetu ana tatizo,’ anaeleza.

Mchezo wa voliboli unapaswa kuchukuliwa kwa uzito katika jamii na haswa miongoni mwa watu walio na umri mkubwa. Wanawake pia wanapaswa kuukumbatia mchezo huu ili kukuza vipawa vyao vya kucheza mchezo wa voliboli na pia kwa lengo la kufanya mazoezi.

Source: Kenya News Agency